Mfanyabiashara mashuhuri nchini na barani Afrika, Said Salim Bakhresa, ameendelea kutajwa kama mmoja wa watu wanaoheshimika zaidi kutokana na mchango wake mkubwa katika maendeleo ya jamii, kukuza uchumi na kutoa ajira kwa maelfu ya watu kupitia makampuni yake mbalimbali.
Bakhresa amefanikiwa kutwaa tuzo kadhaa nyingi za heshima za ndani na nje ya Tanzania, ikiwemo tuzo ya Lifetime Achievement Awards iliyotolewa mwaka 2025 na Kariakoo Business Awards katika Hafla ya tuzo hizo iliyofanyika Mlimani City Jijini Dar es salaam ikiwa ni kutambua mchango wake mkubwa katika maendeleo ya biashara na uchumi wa taifa hili.
Mbali na mafanikio ya kiuchumi, mchango wake katika jamii kupitia uwekezaji, utoaji wa ajira na ushiriki katika shughuli za kijamii umeendelea kumfanya kuwa mfano wa kuigwa kwa wafanyabiashara wengi, hususan vijana wanaoingia katika sekta ya ujasiriamali.
Akizungumza kuhusu safari ya mafanikio yake katika mahojiano na mwandishi wa habari, Bakhresa alieleza kuwa mafanikio hayaji kwa bahati bali yanahitaji bidii, nidhamu na kujitolea kwa kiwango cha juu.
“Muhimu ni kujitahidi kufanya kazi kwa bidii, maana nilikuwa nafanya kazi masaa 24 kwa siku. Sikuwa na starehe ya aina yoyote; maisha yangu yalikuwa ni kazi na nyumbani,” alisema Bakhresa.
Tuzo ya Lifetime Achievement Awards imetajwa kuwa heshima kubwa kwa safari ndefu ya ujasiriamali wa Bakhresa, huku ikiendelea kuwahamasisha wafanyabiashara wengine kujikita katika bidii, uadilifu na kutoa mchango chanya kwa jamii na taifa kwa ujumla.


0 Comments