Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia masuala ya Afya, Mheshimiwa Jafari Seif, ameridhishwa na utekelezaji wa miradi ya afya inayotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Mheshimiwa Jafari Seif ametoa kauli hiyo leo tarehe 7 Februari 2026 wakati wa ziara yake ya kikazi katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, ambapo ametembelea na kukagua ujenzi wa Kituo cha Afya Mchikichini, kukagua eneo la ujenzi wa Kituo cha Afya Buguruni Mtaa wa Mivinjeni pamoja na Kituo cha Afya Mzinga.
Akizungumza mara baada ya ukaguzi huo, Mheshimiwa Jafari Seif amesema ameridhishwa na kasi na ubora wa utekelezaji wa miradi hiyo, akieleza kuwa miradi hiyo ina mchango mkubwa katika kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.
“Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, iko tayari kuendelea kuleta fedha katika miradi mikubwa ya afya kama hii ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya karibu na maeneo yao,” amesema Mheshimiwa Jafari Seif.
Amewapongeza viongozi wa Halmashauri pamoja na watendaji kwa mshikamano wao katika kusukuma mbele utekelezaji wa miradi ya afya kwa manufaa ya wananchi, akisisitiza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutapunguza umbali wa wananchi kufuata huduma za afya na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma hizo.







0 Comments