Dar es Salaam, Februari 9, 2026 —
Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mhe. Paulo Makonda, amesema Serikali ipo katika hatua za mwisho za kufanya mazungumzo na Wizara ya Fedha ili kuweka vivutio maalum vitakavyolenga maendeleo ya watoto kupitia michezo, hatua inayolenga kukuza vipaji vya vijana na kuimarisha sekta ya michezo nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, Mhe. Makonda alisema Serikali imedhamiria kuifanya michezo kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa kwa kuanzia na mtoto, akibainisha kuwa mafanikio ya michezo ya baadaye huanzia katika malezi sahihi ya vipaji vya watoto.
“Tunaangalia namna ya kukaa na Wizara ya Fedha kuona kwa jinsi gani wanaweza kuweka vivutio kwa ajili ya mtoto, ili kuhakikisha vipaji vinatambuliwa mapema, vinathaminiwa na vinapewa mazingira bora ya kukua,” alisema Mhe. Makonda.
Waziri huyo alieleza kuwa Serikali inaendelea kutengeneza mazingira rafiki kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika michezo, akisisitiza kuwa sekta hiyo ina mchango mkubwa katika ajira, uchumi na kuimarisha afya ya jamii.
“Tunatengeneza mazingira bora ili wawekezaji waweze kuwekeza kwenye michezo. Michezo ni biashara, ni ajira na ni utambulisho wa taifa.
Wapenzi wote wa michezo na wawekezaji wana nia njema tunawaalika waje Wizarani tukae, tuzungumze na kuweka mikakati ya pamoja,” aliongeza.
Makonda alibainisha kuwa Serikali haitaki kuona michezo ikibaki kama burudani pekee, bali iwe sekta yenye mifumo madhubuti ya uwekezaji, inayotoa faida kwa wawekezaji na manufaa kwa Watanzania.
Katika hatua nyingine, Mhe. Makonda alitangaza kuwa Rais wa Chama cha Wananchi (CUF) ameridhia kuwasili nchini tarehe 13 Februari, 2026, kwa ziara maalum itakayohusisha mikutano muhimu ya chama hicho.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, Rais huyo wa CUF atafanya mkutano katika Hoteli ya Hyatt Regency, Dar es Salaam, ambapo atakutana na viongozi wa chama hicho katika kikao cha Kamati Tendaji, pamoja na kujadili mipango na mikakati ya chama kwa ngazi ya Afrika nzima kwa mwaka 2026.
Alisema ujio huo unaashiria umuhimu wa Tanzania katika mijadala ya kisiasa na mipango ya maendeleo barani Afrika, sambamba na kuimarisha taswira ya nchi kimataifa.
“Tanzania inaendelea kuwa kitovu cha mikutano muhimu ya kitaifa na kimataifa, na Serikali itaendelea kuhakikisha mazingira ya amani na utulivu yanadumishwa,” alisisitiza Mhe. Makonda.

0 Comments