Dar es salaam
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amesema kuwa ushirikiano wa karibu kati ya Taasisi za Elimu na Waajiri ni nyenzo muhimu ya kuhakikisha vijana wanapata ujuzi unaohitajika katika soko la ajira, ndani na nje ya nchi.
Kauli hiyo imekuja wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Ushirikiano kati ya Taasisi za Elimu na Waajiri, uliofanyika leo, tarehe 09/02/2026, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam
Amesema kupitia mpango huo, sekta binafsi inashiriki moja kwa moja katika kuchangia maendeleo ya elimu, kwa kufadhili tafiti, kusaidia ufadhili wa wanafunzi na kushiriki katika uundaji wa mitaala inayokidhi mahitaji halisi ya soko la ajira.
“Viwanda haviwezi kukua bila nguvukazi yenye ujuzi, na vyuo visiwe visiwa vya nadharia pekee. Ushirikiano huu unahakikisha vijana wanapewa ujuzi unaohitajika sasa na siku za mbele, hususan katika fani za sayansi, teknolojia, ubunifu, tiba, uhandisi na hesabu,” alisema Balozi Dkt. Nchimbi.
Aidha, Makamu wa Rais ametoa wito kwa Taasisi za Elimu na Sekta Binafsi kushirikiana kwa karibu katika kubaini ujuzi muhimu, kuhakikisha vijana wanakuwa tayari kushindana katika soko la ajira la kimataifa.
Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeweka kipaumbele cha kukuza ujuzi, stadi, maarifa na sifa za kuajirika au kujiajiri miongoni mwa wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu, ili maendeleo ya taifa yaende sambamba na rasilimaliwatu iliyoelimika.
Uzinduzi huo wa mpango wa ushirikiano uliohudhuriwa na viongozi wa Serikali, Bunge, viongozi wa dini, waajiri, wakuu wa taasisi na wanafunzi, unalenga kuimarisha uhusiano kati ya elimu na uzalishaji mali, hususan katika sekta za nishati, TEHAMA na viwanda vya kuongeza thamani.



0 Comments