Mkurugenzi wa Wedding Trade Fair, Anna Lema, ametangaza rasmi ujio wa maonesho makubwa ya biashara yanayolenga kuonesha huduma mbalimbali za sherehe, hususan sekta ya harusi na matukio maalum.
Akizungumza pamoja na timu yake inayojumuisha Meneja wa Mahusiano kwa Umma na wawakilishi kutoka soko la kimkakati la Afrika Mashariki (EALC – Ubungo), amesema lengo ni kufungua ukurasa mpya kwa watoa huduma za sherehe na kuwapa nafasi ya kuonesha kazi zao kwa kiwango kikubwa zaidi.
Maonesho hayo yanatarajiwa kufanyika mwezi wa nne (Aprili) mwaka huu, yakileta pamoja wapambaji, wapishi, ma-makeup artist, wabunifu wa mavazi (designers), waandaaji wa juice na cocktail, pamoja na wataalamu wa maandalizi ya gauni la harusi.
Kwa mwaka huu, waandaaji wametoa ofa maalum kwa washiriki. Bei ya banda imepunguzwa hadi shilingi laki 4 tu badala ya laki 7, ikiwa ni kifurushi cha siku tatu kamili za maonesho. Aidha, meza itapatikana kwa shilingi laki moja na nusu tu.
Katika maonesho hayo, wageni watapata nafasi ya kushuhudia moja kwa moja jinsi gauni la harusi linavyoandaliwa, ubunifu wa mapambo, pamoja na huduma mbalimbali za kisasa za sherehe.
Habari njema zaidi ni kwamba kiingilio kitakuwa bure kwa wote, hatua inayolenga kuwapa fursa Watanzania wengi zaidi kushiriki, kujifunza na kufanya maamuzi sahihi kwa maandalizi ya sherehe zao.
Bibi harusi na bwana harusi watarajiwa wamehimizwa kutokukosa tukio hilo muhimu litakalowapa mawazo mapya, ubunifu wa kisasa na huduma bora kwa siku yao maalum.
Waandaaji wamewataka watoa huduma kujitokeza mapema kulipia mabanda na meza zao ili kunufaika na ofa hiyo maalum.
Karibuni sana kwenye Wedding Trade Fair 2026 — kiingilio ni bure, fursa ni kubwa zaidi.

0 Comments