ULEGA ATANGAZA NEEMA KWA WAHANDISI VIJANA

 







Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ametangaza mkakati kabambe wa kukuza ubunifu wa wahandisi wa ndani kwa kuahidi kuzawadia mawazo ya kibunifu yatakayotatua changamoto zilizopo nchini. 


Akizungumza na Jumuiya ya Wanafunzi wa Fani za Uhandisi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) leo, Ulega amesema mpango huo utahusu wanafunzi wanaosomea taaluma hizo katika vyuo vikuu vilivyopo nchini. 


Ulega alisema mtazamo wa wizara yake sasa  ni kuchochea kada ya wanafunzi wasomi wa uhandisi (mainjinia) ambao watakuwa wanajali zaidi kwenye kutatua kero za taifa lao na si kuwa na maandishi mengi yasiyo na mchango kwenye utatuzi wa changamoto. 


Katika mkutano huo ulioandaliwa na Ndani ya Uhandisi na Teknolojia (CoET), Ulega alitangaza zawadi ya shilingi milioni 10 itakayogawanywa kwa washindi watatu waliotoa mawazo bora yatakayosaidia jamii zetu. 


Pia, washindi hao watasaidia kusajiliwa katika Bodi za Kitaaluma, gharama za kufungua kampuni na kupewa mkataba na serikali wa kufanyia kazi wazo lao. 


Alisema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan tayari imeahidi kutoa shilingi bilioni 200 kusaidia makundi ya vijana na wanawake na kwamba mpango huu wa wizara yake ni sehemu ya kuongezea kile kilichoanzishwa kwenye uwezeshaji wa makundi hayo. 


Katika mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Maktaba wa UDSM, Ulega pia aliwatia moyo wanafunzi hao kuwa Tanzania ni Taifa linalotoa fursa sawa kwa wote na kwamba mtu mwenye juhudi na maarifa anaweza kuwa yeyote - akitoa mfano wa Yeye mwenyewe ambaye alikuwa mwanafunzi wa UDSM miaka 20 tu iliyopita lakini sasa amepanda hadi kufika alipo. 


Waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mkuranga, alitumia pia mkutano huo kuzungumzia masuala mbalimbali ya kitaaluma ikiwepo changamoto za teknolojia ya Akili Mnemba (AI). 


Akizungumza kabla ya Mhe Waziri, Mkuu wa Ndaki ya CoET, Dkt. Innocent Macha, alisema kada ya wahandisi imekuwa na mchango muhimu kwa taifa, akitoa mfano wa ushiriki wao katika miradi  mbalimbali ya ujenzi nchini. 


Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa UDSM (Taaluma), Prof. Rose Upor, alimpongeza Waziri Ulega kwa kukubali kuzungumza na jumuiya ya wanafunzi na kueleza kuhusu mwelekeo wa nchi.



Post a Comment

0 Comments