Janeth Rithe: MARCH KUWA MWEZI WA MAOMBOLEZO NA KUMBUKUMBU NCHINI

 



Mwenyekiti wa Ngome ya Wanawake wa ACT Wazalendo, Janeth Rithe, amesema mwezi ujao utaadhimishwa kwa heshima kubwa Tanzania Bara na Zanzibar, ukiwa ni mwezi wa maombolezo na kumbukumbu.

Akizungumza na waandishi wa habari Februari 26, 2026 katika makao makuu ya ACT Wazalendo jijini Dar es Salaam, Rithe alisema chama hicho kitazindua rasmi mnara wa kumbukumbu kwa heshima ya mashujaa wao.

“Ndugu Watanzania, mwezi huu tutaadhimisha kwa heshima kubwa Bara na Zanzibar. Tutazindua mnara rasmi wa kumbukumbu wa shujaa wetu. Tunawaambia watawala kuwa hatuwezi kunyamaza mpaka haki itakapotendeka. Mara zote hatupaswi kukata tamaa. Mungu aiponye Tanzania, taifa la wote,” alisema.

Aliongeza kuwa mwezi mzima wa tatu utakuwa wa maombolezo na kumbukumbu, ambapo kutafanyika ibada ya maombi ya kitaifa Machi 8 kwa ajili ya kuwaombea marehemu wote wapumzike kwa amani.

Aidha, chama hicho kitatembelea wazee kama ishara ya kuthamini hazina ya hekima waliyonayo, kuwafariji yatima waliobaki baada ya matukio ya Oktoba 29 yaliyoacha watoto wengi bila wazazi, pamoja na kufanya usafi na kutoa misaada katika vituo vya afya kama ishara ya shukrani kwa wauguzi.

Rithe pia alibainisha kuwa watachangia damu ili kuokoa maisha ya Watanzania, kuzuru makaburi ya ndugu waliopoteza maisha kikatili, na kufanya mikutano mikubwa ya hadhara nchi nzima.

Alisisitiza kuwa shughuli zote zitafanyika kwa heshima na unyenyekevu, huku wakiahidi kutosahau na kuendelea kudai haki.

Post a Comment

0 Comments