AIRTEL MONEY YAONGEZA KASI YA UJUMUISHI WA FEDHA NA UWEZESHAJI WA KIUCHUMI KWA MAMA LISHE



Airtel Tanzania imethibitisha upya dhamira yake ya kuimarisha ujumuishi wa kifedha na uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake, ikilenga zaidi wajasiriamali wadogo wa chakula wanaojulikana kama Mama Lishe.

Akizungumza Aprili 25, 2026, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Airtel Money, Meneja wa Uhusiano wa Kimkakati wa Airtel Tanzania, Jemima Masimba, alihutubia wadau wakati wa msimu wa tatu wa mpango wa “Empowering Mama Lishe” uliofanyika katika ukumbi wa Ubungo Plaza.

Hafla hiyo iliwakutanisha wawakilishi wa serikali, washirika wa maendeleo pamoja na wanawake wajasiriamali, akiwemo Mbunge wa Viti Maalum anayewakilisha vijana, Mhe. Zainab Abdallah Issa.

Masimba alisema Airtel Money inaendelea kubuni zana bunifu zinazowasaidia wajasiriamali kuweka akiba kwa usalama na kurahisisha miamala katika biashara ndogo ndogo. Alisisitiza umuhimu wa huduma ya Lipa Namba, akibainisha kuwa inawawezesha wanawake kupokea malipo kidijitali na kuhifadhi mapato yao kwa usalama zaidi.

Aidha, alieleza kuwa kumbukumbu za miamala ya kidijitali zinawasaidia wanawake kujenga wasifu wa kuaminika kifedha (financial credibility), jambo muhimu katika kupata mikopo.

“Tunafahamu kuwa wanawake wengi wajasiriamali wanakabiliwa na changamoto ya kukosa dhamana za kupata mikopo rasmi. Kupitia Lipa Namba, historia ya miamala sasa inaweza kutumika kama kigezo cha uaminifu wa kifedha, na hivyo kuwawezesha kupata mikopo kulingana na mzunguko wa fedha zao,” alisema Masimba.

Masimba aliongeza kuwa uwekezaji wa Airtel Tanzania katika kukuza ujuzi kupitia ushirikiano wake na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kupitia mfumo wa VSOMO, unatoa kozi mbalimbali za ufundi ikiwemo za mapishi.

“Uwezeshaji wa kiuchumi hauishii kwenye upatikanaji wa fedha pekee; unahitaji pia maarifa na ujuzi. Tunawahimiza wanawake na vijana kuchangamkia fursa hizi ili kukuza na kuimarisha biashara zao,” alisisitiza.

Baadhi ya washiriki walieleza namna mpango huo ulivyobadilisha maisha yao. Joyce Mmasi wa kikundi cha Bucha Catering Group alisema mpango huo umewawezesha kutoka kufanya biashara kwa kujitegemea hadi kuungana na kufanya kazi kwa vikundi vyenye mpangilio.

“Tulikuwa tumetawanyika, kila mmoja akijitahidi kivyake, hadi Sarrah Ngoma alipotuunganisha,” alisema Joyce. Aliongeza kuwa msaada wa mitungi ya gesi umeboresha mazingira ya kazi na kupunguza utegemezi wa mkaa na kuni.

Kwa upande wake, Amina Abdallah wa kikundi cha Stakishari, mjane anayejishughulisha na biashara hiyo, alisema imekuwa mkombozi kwake kiuchumi.

“Kupitia biashara hii ya Mama Lishe, nimefanikiwa kujenga na kumudu gharama za elimu ya mwanangu,” alisema.

Mgeni Rasmi, Mhe. Zainab Abdallah Issa, alitoa wito wa kuwaunganisha Mama Lishe katika mifumo rasmi ya uchumi, ikiwa ni pamoja na kuwapatia mafunzo ya kushiriki katika zabuni za serikali.

“Nitahakikisha wataalamu kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) wanakuja kutoa mafunzo na kuwaunganisha wanawake hawa kwenye mfumo rasmi wa manunuzi ya umma,” alisema.

Akihitimisha, Masimba aliwahimiza wanawake kuwa na nidhamu ya kuweka akiba kwa kutumia huduma za kidijitali za Airtel Money kama vile Airtel Vikoba. Alibainisha kuwa matumizi ya fedha taslimu mara nyingi husababisha matumizi yasiyo na mpangilio, huku pia akisisitiza umuhimu wa kutumia Lipa Namba kwa usalama zaidi na kuepuka hatari za kubeba fedha taslimu pamoja na tahadhari dhidi ya utapeli.

Post a Comment

0 Comments