Addis Ababa, Ethiopia – Aprili 27, 2026 – Mkurugenzi Mtendaji wa UONGOZI Institute, Kadari Singo, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kuendeleza maendeleo endelevu na kuimarisha uongozi barani Afrika.
Akizungumza katika mkutano wa kikanda uliofanyika Addis Ababa, Singo amepongeza ushirikiano unaoendelea kati ya taasisi hiyo na wadau wa kimataifa, akibainisha kuwa umekuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza mijadala ya kisera, kuimarisha taasisi na kukuza maendeleo jumuishi barani Afrika.
Ametaja pia mafanikio ya mkutano kama huo uliofanyika mwaka jana mjini Kampala, akieleza kuwa umeweka msingi imara wa majadiliano yanayoendelea katika Jukwaa la 12 la Kikanda la Maendeleo Endelevu Afrika.
“Tunathamini ushirikiano tuliojenga na tunaendelea kushukuru kwa msaada wa wadau wetu. Ushirikiano huu unaakisi dhamira ya pamoja ya kuunda mustakabali wa maendeleo ya Afrika kupitia mazungumzo yenye tija na ushirikiano,” amesema Singo.
Aidha, ameipongeza Serikali ya Ethiopia kwa maandalizi mazuri ya mkutano huo pamoja na kuwezesha ushiriki wa wadau mbalimbali wakiwemo vijana, watunga sera, sekta binafsi na asasi za kiraia, akisisitiza kuwa ushirikishwaji wa makundi yote ni muhimu katika kufanikisha maendeleo endelevu.
Singo ameeleza kuwa Afrika ipo katika hatua muhimu inayohitaji uongozi thabiti, sera bora na usimamizi makini wa rasilimali, hususan madini mkakati, ili kuchochea ukuaji wa viwanda, ajira na uchumi wa kijani.
Amefafanua kuwa UONGOZI Institute ni taasisi ya kikanda ya kuendeleza uongozi inayofanya kazi chini ya Ofisi ya Rais wa Tanzania, iliyoanzishwa mwaka 2010 kwa ushirikiano na Serikali ya Finland kwa lengo la kuandaa viongozi wenye uwezo wa kuleta suluhisho jumuishi kwa changamoto za maendeleo barani Afrika.
Kwa mujibu wa Singo, taasisi hiyo hutekeleza majukumu yake kupitia mafunzo ya uongozi, mijadala ya kisera, tafiti na ushauri wa kitaalamu kwa serikali na taasisi mbalimbali, huku ikilenga kujenga uwezo wa viongozi na kuimarisha mifumo ya utawala bora.
Ameongeza kuwa kupitia ushirikiano na taasisi mbalimbali kama African Union, European Union na United Nations Economic Commission for Africa (UNECA), taasisi hiyo imechangia kuimarisha usimamizi wa rasilimali za Afrika ili ziweze kuwanufaisha wananchi moja kwa moja.
Singo amehitimisha kwa kusisitiza kuwa mustakabali wa Afrika unategemea ushirikiano, uongozi wenye maono na uwezo wa kukabiliana na changamoto za dunia ikiwemo mabadiliko ya tabianchi na mabadiliko ya kiuchumi.
Mkutano huo unaendelea kuwa jukwaa muhimu linalowakutanisha viongozi, wataalamu na wadau mbalimbali kujadili na kubuni mikakati ya kukuza maendeleo endelevu na jumuishi barani Afrika.


0 Comments