Serikali ya Tanzania imeendelea kuimarisha miundombinu ya kidijitali baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuzindua rasmi minara 758 ya mawasiliano, ikiwa ni sehemu ya mpango mpana wa kupanua huduma za mawasiliano na kuharakisha uchumi wa kidijitali nchini.
Uzinduzi huo umeenda sambamba na utoaji wa tuzo kwa kampuni za mawasiliano, ambapo Airtel Tanzania pamoja na Vodacom Tanzania, Yas, TTCL na Halotel zilitambuliwa kwa mchango wao katika huduma za kidijitali. Hafla hiyo ilifanyika jijini Dodoma.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Samia alisema kuwa mradi huo umefanikiwa kuongeza au kuboresha huduma za mawasiliano kwa zaidi ya wananchi milioni 8.5 katika vijiji 1,400, hatua inayodhihirisha mafanikio makubwa ya serikali katika kupunguza pengo la kidijitali.
“Leo hii mawasiliano si anasa, bali ni daraja la fursa,” alisema Rais Samia, akisisitiza kuwa serikali itaendelea kuwekeza katika sekta ya TEHAMA chini ya Dira ya 2050 na Ilani ya CCM ya mwaka 2025.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Charles Kamoto, alipokea tuzo kwa niaba ya kampuni hiyo na kueleza kuwa mradi huo ni ushahidi wa mafanikio ya ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi katika kukuza mawasiliano nchini.
Alisema minara hiyo si tu miundombinu, bali ni nyenzo muhimu zinazowaunganisha wananchi katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, elimu na biashara ndani ya uchumi wa kidijitali.
Taarifa zinaonyesha kuwa kati ya minara 758 iliyozinduliwa, Airtel Tanzania imejenga minara 169 kupitia mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi, huku UCSAF ikitoa takriban shilingi bilioni 126 kusaidia ujenzi huo katika maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara.
Kwa sasa, Airtel Tanzania ina zaidi ya vituo 3,700 vya mtandao vyenye huduma za 4G, huku upanuzi wa 5G ukiendelea katika baadhi ya mikoa. Kampuni hiyo pia imeweka zaidi ya kilomita 3,700 za mkongo wa nyaya za mawasiliano (fiber optic) na kuhudumia zaidi ya watumiaji milioni 23 nchini.
Katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2025, Airtel Tanzania imewekeza zaidi ya dola milioni 316 katika miundombinu, kulipa kodi na tozo mbalimbali zinazofikia trilioni 1.69 za shilingi za Kitanzania, pamoja na kurejesha gawio la shilingi bilioni 289 kwa serikali.
Rais Samia alieleza kuwa uamuzi wa serikali kusimamia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano unalenga kuboresha uratibu wa miundombinu ya kimkakati, huku akielekeza Wizara ya Mawasiliano kuhakikisha huduma za intaneti zinafika hadi vijijini na vitongojini.
Alisisitiza pia umuhimu wa kulinda miundombinu ya mawasiliano pamoja na kuzingatia maadili ya kitaifa katika matumizi ya teknolojia.
Hatua hiyo inaonesha dhamira ya Tanzania kujenga uchumi imara wa kidijitali, kuongeza ujumuishaji wa kifedha, na kujiimarisha kama kitovu cha TEHAMA katika ukanda wa Afrika Mashariki.



0 Comments