Dar es Salaam – Kampuni ya Umoja Movies Distribution leo Aprili 23, 2026 imemtambulisha rasmi msanii wa filamu Duma kuwa balozi wake, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za kampuni hiyo zilizopo Ilala Sharifu Shamba, ndani ya jengo la Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), kwenye chuo cha uandishi wa habari cha DSJ jijini Dar es Salaam.
Katika hafla hiyo, Duma pia alisaini rasmi mkataba wa ushirikiano na Umoja Movies, hatua inayolenga kupanua wigo wa burudani pamoja na kuongeza fursa za kipato kwa wasanii wa filamu nchini.
Akizungumza wakati wa utiaji saini huo, mwakilishi wa Umoja Movies amesema kampuni hiyo inalenga kujenga jukwaa pana la burudani linalojumuisha sekta mbalimbali ikiwemo filamu, muziki na maudhui ya kidijitali, huku wakilenga kuwafikia watu wengi zaidi kupitia teknolojia za kisasa.
Amesema huduma zao zinapatikana kupitia simu za mkononi, jambo linalowawezesha watumiaji kupata burudani na ujumbe kwa urahisi zaidi, huku pia likiwa chanzo cha ajira kwa vijana kupitia nafasi mbalimbali kama mawakala na wasambazaji wa maudhui katika maeneo tofauti nchini.
“Tumelazimika kupanua wigo kwa kushirikisha watu wa kada tofauti, siyo wasanii wa filamu tu, bali pia DJs na baadaye wanamuziki. Lengo ni kujenga jukwaa la burudani linalotoa ajira na kipato,” amesema mwakilishi huyo.
Kwa upande wake, Duma ameishukuru kampuni hiyo kwa kumpa nafasi ya kuwa balozi, akieleza kuwa ni hatua kubwa katika safari yake ya sanaa na kwamba ataendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha anatimiza malengo ya ushirikiano huo.
Amesema anaamini uzoefu wake pamoja na ushirikiano wa mashabiki wake utasaidia kukuza zaidi soko la filamu na burudani nchini, huku akisisitiza kuwa kujiunga kwake na Umoja Movies hakumaanishi ataacha kufanya kazi nyingine.
“Hii ni fursa ya kuongeza thamani ya kazi zangu na kupata vyanzo vipya vya mapato. Si kwamba ninaacha kazi nyingine, bali ninaongeza wigo wa kazi,” amesema Duma.
Ushirikiano huo unatarajiwa kuongeza ushindani katika tasnia ya burudani nchini, huku ukiwapa wasanii nafasi zaidi ya kunufaika na majukwaa ya kidijitali na kufikia hadhira pana zaidi ndani na nje ya Tanzania.
.webp)
.webp)

0 Comments