DKT. JAFAR SEIF AWATAKA MAAFISA LISHE KUONGEZA JUHUDI KUPAMBANA NA LISHE DUNI

 




Dodoma – Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Jafar Seif, amewataka Maafisa Lishe nchini kuongeza jitihada katika kukabiliana na changamoto za lishe na magonjwa yanayotokana na lishe duni, akieleza kuwa hali ya lishe bado si ya kuridhisha.

Akihutubia Mkutano wa Mwaka wa Uratibu wa Huduma za Lishe uliowakutanisha Maafisa Lishe kutoka halmashauri zote 184 na mikoa 26 ya Tanzania Bara jijini Dodoma, Dkt. Seif alisema hatua za haraka zinahitajika kubadili mwenendo wa viashiria vya lishe nchini.

Amebainisha kuwa kati ya watoto 10 wenye umri chini ya miaka mitano, watatu wanakabiliwa na udumavu huku asilimia 58 wakikumbwa na upungufu wa damu. Aidha, tatizo hilo linaathiri pia asilimia 56 ya wanawake wajawazito na asilimia 42 ya wanawake wenye umri wa kuzaa (miaka 15–49).

Kwa upande wa uzito uliopindukia, amesema asilimia 36 ya wanawake wenye umri wa miaka 20–49 wanakabiliwa na hali hiyo, huku wanaume wakiwa asilimia 17, jambo linalochangia kuongezeka kwa magonjwa sugu yasiyoambukizwa kama Kisukari, Shinikizo la damu na magonjwa ya moyo.

Dkt. Seif aliwataka wataalamu wa lishe kuongeza uwajibikaji katika utekelezaji wa afua mbalimbali ili kufikia mabadiliko yanayohitajika, huku akisisitiza umuhimu wa kuboresha takwimu, kuimarisha mpango wa chakula mashuleni na kusimamia utekelezaji wa kanuni za uongezaji wa virutubisho kwenye vyakula.

Aidha, amesema serikali imeendelea kuongeza uwekezaji katika sekta ya lishe, ambapo bajeti imeongezeka kutoka shilingi bilioni 2 mwaka wa fedha 2017/2018 hadi kufikia bilioni 20.3 mwaka 2025/2026.

Katika kuimarisha huduma, Dkt. Seif amesema serikali imeajiri Maafisa Lishe 654 waliopangiwa katika mikoa na mamlaka za serikali za mitaa kote nchini ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa mipango ya lishe.

Amesisitiza kuwa juhudi za pamoja zinahitajika ili kupunguza athari za matatizo ya lishe na kuboresha afya ya wananchi kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments