Airtel Africa imetangaza ongezeko kubwa la mapato na faida kwa mwaka ulioishia Machi 31, 2026, likichochewa zaidi na matumizi ya intaneti (data) na huduma za Airtel Money.
Kampuni hiyo imesema faida halisi imepanda zaidi ya mara mbili hadi dola milioni 813, huku mapato yakiongezeka kwa asilimia 29.5 kufikia dola bilioni 6.42.
Ukuaji huo umechangiwa na ongezeko la wateja, ambapo jumla imefikia milioni 183.5, pamoja na matumizi makubwa ya data na huduma za kifedha kidijitali.
Huduma ya Airtel Money imeendelea kukua kwa kasi, ikiwa na wateja milioni 54.1 na ongezeko la miamala kufikia zaidi ya dola bilioni 215 kwa mwaka. Wakati huo huo, matumizi ya data kwa kila mteja yamepanda hadi GB 8.9 kwa mwezi.
Mkurugenzi Mtendaji Sunil Taldar amesema mafanikio hayo yanatokana na uwekezaji katika mtandao, upanuzi wa huduma za kidijitali na ufanisi wa uendeshaji.
Airtel Africa pia inaendelea kupanua miundombinu yake, ikijumuisha uwekezaji wa zaidi ya dola milioni 884 na mpango wa kuongeza uwekezaji hadi dola bilioni 1.1 ifikapo 2027.
Kampuni hiyo imesema mustakabali wake unategemea zaidi ukuaji wa huduma za data na fedha za kidijitali, ambazo sasa ni injini kuu ya mapato barani Afrika.

0 Comments