Mbunge wa Jimbo la Chalinze na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete amehimiza watumishi wa umma kuendelea kuimarisha uwajibikaji, ushirikiano na utoaji wa huduma bora ili wananchi wapate huduma zenye tija na Serikali itimize malengo yake ya maendeleo.
Kikwete ameyasema hayo Julai 24, 2026 kwenye Makao Makuu ya Halmashauri ya Chalinze alipokutana kufanya mkutano na watumishi wa Halmashauri ya Chalinze kuanzia Wakuu wa Idara na Vitengo wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Ndugu Ramadhani Possy, wakuu wa taasisi za umma Chalinze, madiwani, Maafisa Tarafa na Watendaji Kata na Vijiji.
Kwenye Kikao Kazi hi hicho, Kikwete amesisitiza kuwa watumishi wa umma ni nguzo muhimu katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali hivyo wanapaswa kutekeleza wajibu wao kwa uadilifu, weledi na uwajibikaji wakizingatia Katiba, sheria, kanuni na maadili ya utumishi wa umma.
Aidha, amesema utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 pamoja na Mipango ya Maendeleo ya muda wa kati na mrefu unategemea utendaji bora wa watumishi wa umma, huku akibainisha kuwa ushirikiano kati ya watendaji na viongozi wa siasa ni muhimu katika kuhakikisha miradi na huduma zinawafikia wananchi kwa ufanisi.
Vilevile, Kikwete amewataka watumishi kutumia kikamilifu mifumo ya kidijitali ya serikali katika kusimamia utendaji wao, kupata taarifa za kiutumishi na kutatua changamoto kwa wakati.
Alihitimisha, kwa kuwataka watumishi wa umma kuendelea kujenga imani ya wananchi kwa serikali kupitia uwajibikaji, uadilifu, usimamizi mzuri wa rasilimali za umma na utoaji wa huduma bora.



.jpg)
0 Comments