WAZIRI ANGELLAH KAIRUKI: MPWAPWA KUNUFAIKA NA MINARA 57 ITAKAYOBORESHA HUDUMA ZA MAWASILIANO,RC SENYAMULE AWAHAKIKISHIA JUHUDI ZA SERIKALI KUTEKELEZA MIRADI MINGINE MUHIMU WILAYANI HUMO










Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, amesema Serikali inatekeleza mradi wa kupeleka minara ya kurahisisha huduma za mawasiliano katika maeneo tisa ya Wilaya ya Mpwapwa yenye changamoto hiyo ambapo mpaka sasa tayari imepeleka minara 57 kwenye Kata 28 ambayo imesaidia kutatua changamoto hiyo.


Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya Mlembule, Wilaya ya Mpwapwa katika viwanja vya shule ya msingi Mlembule wakati wa ziara yake ya kikazi iliyokwenda sambamba na ukaguzi wa miradi ya maendeleo Julai 23, 2026, Waziri Kairuki alisema;


*“Kwa upande wa Wilaya ya Mpwapwa, tayari tumekwishaleta minara takribani 57 na mna mawasiliano takribani Kata 28, zimebakia Kata 5, vile vile, tuna mradi ambao tunautekeleza wa takribani shilingi Bilioni 1.6 ambao Dodoma tutaleta minara 14, lakini pia kwa upande wa Wilaya ya Mpwapwa, kuna Kata ya Ipera kwenye Kijiji cha Kikuyu, kata ya Masa katika Kijiji cha Mkoleko na kwenyewe pia tutahakikisha tunaleta minara”.*


Aidha, aliongeza kuwa, Serikali inafanya jitihada hizo kwa kuwa huduma za mawasiliano kwa sasa si anasa bali ni ya lazima kutokana na kutumika katika kila sekta hususan za afya, elimu, kilimo na fedha kwa kuwa inatumia mifumo ya kiteknolojia kusomana ili kuweza kutoa huduma za kijamii.


Vile vile, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule alisema Serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha wananchi wanafikiwa na huduma za maji safi na salama kwa kuleta miradi kadhaa ya maji katika Kata hiyo ikiwa ni pamoja na uchimbaji wa visima viwili katika Vijiji vya Tambi na Mlembule, sanjari na Mradi wa maji katika Kijiji cha Wizele kupitia wadau wa ‘Water for people’ utakaogharimu kiasi cha shilingi Milioni 891.


Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mpwapwa Mhe. George Malima, alisema kuwa kutokana na jitihada za Serikali kuboresha huduma za mawasiliano kwa kuweka minara maeneo mengi ya Nchi, katika Jimbo lake, tatizo hilo limepungua kwa asilimia 80 tofauti na awali kabla ya kuanza kwa mradi wa kuweka minara hiyo.

Post a Comment

0 Comments