KATIBU MPYA TUGHE TAIFA AAHIDI KULETA MAPINDUZI KWA WAFANYAKAZI KATIKA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAO.
Na Victor Masangu, Pwani
Katibu Mkuu mpya wa. Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania TUGHE, Rugemarila Rutatina, amesema hatosita kuwashughulikia viongozi na watumishi wenye tabia ya kuchelewesha majukumu yao ya utendaji katika chama.
Pia Katibu huyo ameesema atalivalia njuga suala la viongozi ambao wanatoa udhuru bila sababu za msingi, huku akisisitiza kuwa kipindi cha visingizio kimekwisha na sasa ni wakati wa utekelezaji wa majukumu kwa vitendo ili kuwatumikia wanachama ipasavyo.
Rutatina ameyabainisha hayo wakati wa hafla hiyo, kubwa ya kukabidhi ofisi kwa uongozi mpya uliochaguliwa hivi karibuni, hafla ambayo imefanyika Makao Makuu ya chama hicho na kuhudhuriwa na viongozi.mbali mbali wastaafu, wanachama kutoka matawi mbalimbali wakiwemo wa Mkoa wa Pwani.
"Kitu kikubwa watendaji na viongozi kuhakikisha wanatimiza majukumu yao ipasavyo na kwamba waweke mikakati ya kuwatumikia wanachama na kwamba atakuwa na msimamo mkali dhidi ya wale uzembe,"amebainisha Katibu huyo.
Kadhalika Katibu huyo amesema kwamba ataendelea kushirikiana na viongozi wenzake na kwamba ataweka malengo makubwa ya kuongeza wanachama na kukiimarisha chama.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taifa wa TUGHE, Aloisi Mapembe, amewataka viongozi wote kutobweteka baada ya kupewa madaraka na badala yake kila kiongozi kwa nafasi yake aweke mkakati mahususi wa kuongeza wanachama angalau 100 kwa mwaka.
Aidha Mwenyekiti huyo ameahidi kwamba katika uongozi wake ataanzisha imiradi mbalimbali ya kiuchumi ya chama itakayowaongezea kipato wanachama na kukifanya chama kujitegemea kiuchumi.
Naye Mwenyekiti wa TUGHE Mkoa wa Pwani, Catherine Katele, amesema uchaguzi umeisha na kilichobaki ni kufanya kazi kwa bidii, akibainisha kuwa wamepewa heshima kubwa na kuaminiwa na wanachama hivyo watahakikisha wanairejesha imani hiyo kwa kutetea maslahi ya wafanyakazi.
Naye Mwakilishi wa wafanyakazi Sara Stephano akiahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na uongozi mpya ili kuleta mabadiliko chanya katika kutetea maslahi ya wafanyakazi wa afya na serikali nchini.


0 Comments