Na Victor Masangu,Kibaha
Karika kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita katika kuboresha sekta ya elimu Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dk. Nicas Mawazo ameahidi kuchangia mifuko 150 ya Saruji kwa lengo la kuendelea kuboresha miundombinu ya majengo katika shule ya awali na msingi ya Finest iliyopo kata ya Mkuza Wilaya ya Kibaha.
Mstahiki meya huyo ameahidi kuchangia mifuko hiyo ya saruji wakati wa sherehe ya mahafali ya wanafunzi wa awali wa shule hiyo kwa ajili ya kuweza kuboresha mazingira ya majengo katika shule hiyo.
Dk.Mawazo amebainisha kwamba ameamua kuchangia mifuko hiyo kutokana na kuguswa na juhudi zinazofanywa na uongozi wa shule hiyo katiba kuboresha sekta ya elimu.
"Nimekuja katika mahafali haya lkn nimejionea uwekezaji ambao umefanyika na nimpongeze kwa dhati mkurugenzi wa shule hii kwa juhudi zake kuwekeza kwa watoto hawa kwani ni kitu cha msingi sana katika suala zima la elimu,"amebainisha Dk.Mawazo.
Pia amesema kuwa anawapongeza wawekezaji kwenye elimu kwani zamani sekta ya elimu ilikuwa inawekezwa na taasisi kubwa lakini kwa sasa wanawekeza hata vijana.
"Elimu ni kila kitu hivyo lazima tuwekeze kwenye elimu kwa kusomesha watoto wetu na hakuna namna lazima tuwekeze ili watoto wasome hadi chuo kikuu kwani elimu ni kitu cha thamani kubwa,"amesema Mawazo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shule hiyo Abubakar Allawi amesema kuwa moja ya changamoto ni miundombinu ya barabara pamoja majengo.
Allawi amesema kuwa lengo la kuanzishwa shule hiyo ni kutoa elimu bora kwa gharama nafuu ili vijana wa Kibaha wawe na elimu bora itakayoendana na wakati.
Aidha Mkurugenzi huyo amesema kwamba wataendelea kushirikiana bega kwa bega na serikali pamoja na wadau wengine katika kuwekeza zaidi katika sekta ya elimu kuanzia ngazi ya awali na kuendelea.

0 Comments