SERIKALI YAENDELEA KUIMARISHA MIUNDOMBINU NA UCHUMI: RAIS SAMIA KUZINDUA MRADI MKUBWA WA MATANKI YA MAFUTA DAR ES SALAAM

 









Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa matanki 15 ya kisasa ya kuhifadhia mafuta kesho tarehe 03 Machi 2026 katika eneo la Mnadani, Kigamboni jijini Dar es Salaam, ikiwa ni hatua muhimu ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha sekta ya uchukuzi na kukuza uchumi wa Taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Uchukuzi Makame Mbarawa amesema mradi huo wenye thamani ya Shilingi bilioni 678.6 ni sehemu ya mpango mpana wa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam unaolenga kuongeza ufanisi, ushindani wa bandari pamoja na kuvutia uwekezaji zaidi nchini.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, matanki hayo yatakuwa na uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo 378,000 za mafuta na yatasaidia kupunguza muda wa meli za mafuta kukaa bandarini kutoka wastani wa siku 10 hadi siku 3, hatua itakayoongeza kasi ya upokeaji na usafirishaji wa mizigo.

Ameeleza kuwa mradi huo unaenda sambamba na ujenzi wa magati mapya yenye urefu wa mita 500 kila moja, yanayolenga kuongeza uwezo wa bandari kufikia kuhudumia zaidi ya tani milioni 60 kwa mwaka.

Katika tathmini ya utendaji wa bandari, Prof. Mbarawa amesema kuanzia Julai hadi Desemba 2025, Bandari ya Dar es Salaam ilihudumia tani milioni 19.9 za mizigo huku Serikali ikiweka malengo ya kufikia tani milioni 40 ifikapo mwisho wa mwaka wa fedha 2025/2026.

Aidha, maboresho hayo yanaendana na mkakati wa Serikali wa kuimarisha usafirishaji wa mizigo kupitia reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) ili kupunguza utegemezi wa barabara, kupunguza ajali, msongamano pamoja na gharama za usafirishaji.

Waziri Mbarawa amesisitiza kuwa sekta ya uchukuzi imeendelea kuwa mhimili mkubwa wa uchumi wa Taifa, ikichangia zaidi ya shilingi trilioni 2.48 kwa mwaka na kutoa ajira zaidi ya milioni tatu hususan katika sekta ndogo ya bandari.

Amesema zaidi ya asilimia 90 ya mizigo inayotoka Bandari ya Dar es Salaam kwa sasa hupitia barabarani hali inayosababisha uchakavu wa miundombinu, ajali pamoja na ucheleweshaji wa mizigo, hivyo Serikali inaendelea kuwekeza kwenye reli na miundombinu mingine ya kisasa ili kuongeza ufanisi wa usafirishaji.

Kwa ujumla, Serikali inalenga kuboresha mazingira ya biashara, kufungua fursa mpya za kiuchumi na kuifanya Tanzania kuwa lango kuu la biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi inatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, wadau wa sekta ya uchukuzi pamoja na wanahabari nchini.

Post a Comment

0 Comments