Waziri wa Uchukuzi, Makame Mbarawa, amesema Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ya kuimarisha sekta ya uchukuzi nchini, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa matanki mapya ya kuhifadhia mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, tarehe 28 February 2026, jijini Dar es Salaam, Mbarawa amesema kuwa kesho, Mungu akijalia, tarehe 03 March, kutafanyika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa matanki 15 ya mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Amesema mradi huo unaonesha dhamira ya kweli ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha miundombinu ya uchukuzi na kuongeza ufanisi wa bandari nchini.
Mbarawa alieleza kuwa ujenzi wa magati na matanki hayo ni sehemu ya mkakati mpana wa kuongeza uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam, ambapo kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kuongeza uwezo wa bandari kufikia tani milioni 90 kwa mwaka.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, katika kipindi cha Julai hadi Desemba, Bandari ya Dar es Salaam ilihudumia tani milioni 19.9 za mizigo, huku matarajio yakiwa kufikia tani milioni 40 ifikapo mwisho wa mwaka wa fedha 2025/2026.
Aliongeza kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa matanki 15 ya kuhifadhia mafuta yenye uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo 378,000, hatua itakayosaidia kupunguza muda wa meli kukaa bandarini kutoka siku 10 za sasa hadi siku tatu baada ya mradi kukamilika.
Mbarawa alisema maboresho hayo yanaenda sambamba na kuimarishwa kwa usafirishaji wa mizigo kwa reli, akibainisha kuwa kwa sasa zaidi ya asilimia 90 ya mizigo inayotoka Bandari ya Dar es Salaam husafirishwa kwa njia ya barabara.
“Matokeo yake barabara zetu zinachakaa haraka, ajali zinaongezeka pamoja na ucheleweshaji wa mizigo na msongamano mkubwa wa magari,” alieleza.
Aidha, alisema sekta ya uchukuzi inaendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi wa Taifa, ikichangia zaidi ya Shilingi trilioni 2.48 kwa mwaka katika mapato ya Serikali, huku ajira zaidi ya milioni tatu zikiendelea kuzalishwa hususan katika sekta ndogo ya bandari.
Waziri Mbarawa aliwashukuru wadau wote wa sekta ya uchukuzi ikiwemo Tanzania Ports Authority (TPA) kwa mchango wao katika maendeleo ya bandari na uchumi wa nchi.
Amesema hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi itafanyika eneo la Mnazi Mmoja, Kigamboni, na amewakaribisha wanahabari pamoja na wadau wote wa usafirishaji kushiriki tukio hilo muhimu.
“Yote tunayoyafanya ni kuboresha ufanisi wa bandari na kufungua zaidi fursa za biashara kwa nchi yetu,” alihitimisha.








0 Comments