MBETO HAMIS MBETO AHIMIZA ELIMU YA QURAN NA AMANI KATIKA MASHINDANO YA KUHIFADHI QURAN DAR ES SALAAM

 



Dar es Salaam, 28 February 2026 – Mbeto Hamis Mbeto amehudhuria kama mgeni rasmi mashindano ya tatu ya kuhifadhi Quran yaliyofanyika leo jijini Dar es Salaam, akisisitiza umuhimu wa elimu ya dini, malezi bora ya watoto na kudumisha amani katika jamii.

Akizungumza mbele ya washiriki wa mashindano hayo, Mbeto Hamis alisisitiza kuwa kujua Quran na kuishi kwa misingi yake kunasaidia mtu kuwa na maisha safi na yenye mafanikio.

"Ukiijua Quran na ukiishi na Quran vizuri, mambo yako yatakuwa safi. Mtoto akielelewa akijua Quran, anakuwa mtoto bora. Na kama mtoto hana Mungu jua, hakuna kitu," alisema Mbeto.

Mbeto pia alihimiza wazee na walimu kuhakikisha watoto wanapewa malezi bora na kuelimishwa kumpenda Mtume Muhammad (SAW). Alieleza kuwa, kwa mujibu wa hadithi sahihi, binadamu anapokufa matendo yake yote hukatika isipokuwa mambo matatu, ikiwemo uwekezaji wa kumlea mtoto awe mwema na amjue Mungu.

"Wazee wenzangu, tuhakikishe tunawafundisha watoto wetu kumpenda Mtume Muhammad. Ukiwekeza hapa, utafaidika," aliongeza.

Aidha, alitambua mchango wa walimu wa madrasa, akisema:

"Ninyi waalimu wa madrasa mnafanya kazi nzuri sana. Hili ni jambo kubwa, nataka nipate hizi fadhila."

Mbeto alisisitiza pia umuhimu wa kudumisha amani:

"Kitu ambacho hatutakiwi kuchezea ni amani. Bila amani hakuna ibada, hakuna chochote ambacho unaweza kufanya. Hivyo, tudumishe amani yetu."

Hotuba ya Mbeto Hamis Mbeto katika mashindano haya inachangia kutoa motisha kwa watoto, walimu na jamii kwa ujumla kuendelea kuhifadhi Quran, kuishi kwa misingi yake na kuhakikisha mshikamano wa kijamii unadumishwa. Mashindano haya yanaendelea leo, huku washiriki wakiendelea kuonyesha umahiri wao katika kuhifadhi Quran.

Post a Comment

0 Comments