Na Victor Masangu,Bagamoyo
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameipongeza kwa dhati serikali ya Mkoa wa Pwani kwa kuendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuendelea kuwa kinara namba moja katika suala zima la uwekezaji katika viwanda mbali mbali.
Waziri mkuu ameyabainisha hayo wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja ya kutembelea katika baadhi ya wawekezaji na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kongani ya Viwanda ya Hongwang Tanzania (HWTZ) SEZ Limited, Bagamoyo.
Aidha, amesisitiza kuwa wananchi waliopisha maeneo kwa ajili ya uwekezaji wanapaswa kulipwa haki zao ili kumaliza malalamiko na migogoro ya ardhi, huku shughuli za uwekezaji zikiendelea katika mazingira ya amani na ushirikiano.
Serikali imeweka chanzo maalumu cha fedha kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi hao, hatua inayolenga kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kupunguza migogoro ya ardhi inayotokana na kuchelewa kwa malipo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Stanslaus Haroon Nyongo, amesema mkoa huo unaendelea kuvutia wawekezaji kutokana na juhudi za kuboresha mazingira ya uwekezaji.
Mkoa wa Pwani una jumla ya viwanda 1,768, vikiwemo vikubwa 503, vya kati 248 na vidogo 1,017, pamoja na kongani 35 za viwanda.


0 Comments