JUMUIYA YA MARIDHIANO YAANIKA FAIDA YA ZIARA ZA DKT ALHAD MUSA NJE YA NCHI.

 Na Mwandishi wetu. Dar es Salaam. 


JUMUIYA ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) imeeleza faida za ziara ya Mwenyekiti wa JMAT Taifa Sheikh Dkt. Alhad Mussa Salum aliyofanya katika Nchi za Korea Kusini, Kenya na Irani.



Faida hizo zimebainishwa na Katibu Mkuu JMAT Taifa Askofu Dkt. Israel Ole-Gabriel Maasa akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 12, 2023 jijini Dar es Salaam.


“Mhe. Mwenyekiti Wetu Taifa Sheikh Dkt. Alhad Mussa Salum alipata mwaliko wa kuhudhuria Mkutano wa Amani wa Kimataifa, uliwahusisha viongozi wa dini na wadau mbalimbali wa Amani kutoka ulimwengunikote. Mkutano huu ulifanyika jijini Seoul nchini Korea Kusini, kuanzia Tarehe 17 hadi 19 Agosti, 2023,” amesema Askofu Dkt. Maasa na kuongeza,




“Mkutano uliandaliwa na Shirika la Kimataifa la Amani lijulikanalo kama Heavenly culture World Peace restoration of Light (HWPL),”.


Amesema katika ziara hiyo Mwenyekiti aliambatana na viongozi wawili wa Kitaifa, Fatma Fredrick Kikkides (Mratibu JMAT Taifa) na Ayoub Joseph Sanga (Mkurugenzi wa Idara Kuu ya Mipango, Fedha, Uchumi na Utekelezaji) kwamba JMAT ilishiriki Mkutano huo kikamilifu na kwa heshima kubwa.


Ametaja faida ambazo JMAT imezipata kutokana na kushiriki Mkutano huo kuwa ni kujenga mahusiano ya Kimataifa na Taasisi ya Kimataifa ya HWPL na kusaini mkataba wa kufanya kazi pamoja na shirika hilo la Kimataifa juu ya masuala ya Amani.


Faida nyingine ni Mratibu wa JMAT Taifa Fatma Fredrick Kikkides kupewa Ubalozi wa Amani duniani kupitia Shirika Tanzu la HWPL linaloshughulikia Amani kwa wanawake liitwalo International Women Peace Group (IWPG) na kukutana na wadau mbalimbali wa Amani duniani na Hivyo kukuza mtandao wa kufanya kazi na Watu wengi duniani kwa ajili ya Amani Duniani.


Askofu Dkt. Maasa ameeleza kuwa katika ziara nchini Korea, Mwenyekiti wa JMAT alipata fursa ya kutembelea makumbusho ya vita ya Korea Kusini na Korea Kaskazini iliyokuwa ni vita kubwa iliyosababisha mauaji ya Watu karibuni milioni nne (4) katika vita iliyodumu kwa miaka mitatu kuanzia Mwaka 1950 hadi 1953.


“Mhe. Mwenyekiti amejifunza kwa kuona athari ya vita na kutambua kwamba vita ni kitu kibaya sana. Hivyo JMAT imepata funzo kwamba kazi tunayoifanya ni kazi kubwa na muhimu sana kwa ajili ya Taifa letu pendwa la Tanzania,” amesema Askofu Dkt. Maasa na kueleza,


“Katika ziara hii ya makumbusho ya vita ya Korea Mwenyekiti aliambatana na Fatma Fredrick Kikkides, Mratibu JMAT Taifa na Balozi wa Amani Duniani wa IWPG pamoja na Ayoub Joseph Sanga, Mkurugenzi Idara ya Kuu ya Mipango, Fedha, Uchumi na Utekelezaji ya JMAT Taifa,”.


Kuhusu ziara ya kikazi nchini Kenya Septemba 26, 2023 baada ya kupata Mwaliko kuwa mgeni rasmi jijini Mombasa katika shughuli ya kumtawaza Mufti Mpya wa Kenya, Sheikh Mshali Khamis Mshali Ashiraazy kupitia Taasisi ya Kemnack nchini Kenya.


Kwamba jambo hilo limeiletea heshima kubwa JMAT na heshima kwa Mwenyekiti pia, kwamba katika safari hiyo Mwenyekiti aliambatana na maafisa kadhaa kutoka Makao Makuu ya JMAT, Dar es Salaam.


Ameendelea kueleza kuwa katika ziara ya nchini Irani, Mwenyekiti wa JMAT Taifa alipata nafasi ya kutoa hotuba juu ya masuala ya Umoja wa Kitaalam na Mahusiano ya Dini mbalimbali.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa JMAT Taifa Sheikh Dkt. Alhad Mussa Salum amesema mkataba waliosaini ni ishara kuwa wanafanya kazi kimataifa katika masuala ya Amani.


Hivyo amewataka Watanzania kuendelea kushirikiana na kuiunga mkono Serikali kuhakikisha Amani inaendelea kuwepo nchini.


Ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutunukiwa Shahada ya heshima ya falsafa nchini India.


Naye Mratibu JMAT Taifa Fatma Fredrick Kikkides amesema atatumia fursa Ubalozi wa Amani Duniani wa IWPG aliopata kutoa elimu ya Amani kwa wanawake.

Post a Comment

0 Comments