Na Mwandishi wetu
Serikali imesema inakusudia kuendelea kuboresha bandari ya Dar Es Salaam lengo likiwa ni kuhakikisha miaka michache ijayo bandari hiyo inakuwa bandari kubwa zaidi kusini mwa jangwa la Sahara.
Hayo yameelezwa leo na Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi Prof. Godius Kahyarara alipokutana na wadau wa bandari nchini katika kikao cha kujadili maboresho ya utendaji wa bandari hiyo jijini Dar Es Salaam.
"Sisi kama serikali tuko kwenye mpango kabambe ni lazima tuongeze Gati kwenye bandari ya Dar Es Salaam, mpaka sasa mikakati inakwenda vizuri na TPA wanafanya vizuri, " Amesema Prof. Kahyarara.
Pia Prof. Kahyarara ametoa wito kwa wadau wa bandari kuwekeza katika bandari zote nchini kadri wanavyoona fursa badala ya kuiachia serikali pekee kufanya u
wekezaji huo kwani bandari zina wateja wa kutosha.Awali akizungumza katika kikao hicho Mkurugenzi wa Bandari ya Dar Es Salaam Abed Gallus amesema katika mwaka wa fedha uliopita 2023/24 shehena katika bandari hiyo iliongezeka kwa asilimia 7.8 huku upande wa makasha ongezeko likiwa ni asilimia 1.
Aidha Gallus amesema kuwa msongamano wa meli zinazosubiri kupakuliwa umeendelea kupungua kila siku huku akibainisha kuwa meli zinazoingia zimeendelea kupungua kufuatia bandari kuwa na uwezo wa kupokea meli kubwa baada ya kuongezwa kwa kina cha bandari hiyo.





0 Comments