MAHAFALI YA 28 YA KITUO CHA UHUSIANO WA KIMATAIFA CHA DKT. SALIM AHMED SALIM (CFR) KUFANYIKA JANUARI 6, 2026

 


Na Mwandishi Wetu

Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim (CFR) kinatarajia kufanya Mahafali yake ya 28 tarehe 6 Januari, 2026, ambapo wahitimu kutoka programu mbalimbali za mafunzo ya diplomasia, uongozi na mahusiano ya kimataifa watatunukiwa vyeti vyao.

Mgeni Rasmi katika mahafali hayo anatarajiwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo, ambaye atahutubia wahitimu, wageni waalikwa pamoja na wadau wa sekta ya diplomasia na uhusiano wa kimataifa.

Mahafali hayo yatakutanisha viongozi wa Serikali, mabalozi, wawakilishi wa taasisi za kimataifa, wahadhiri, wazazi pamoja na wanafunzi kutoka ndani na nje ya nchi, jambo linaloonesha nafasi muhimu ya kituo hicho katika kukuza diplomasia na ushirikiano wa kimataifa.

Akizungumza kuelekea mahafali hayo, uongozi wa kituo hicho umeeleza kuwa Mahafali ya 28 ni hatua muhimu katika kuendeleza dhamira ya kumuenzi Hayati Dkt. Salim Ahmed Salim (CFR) kwa kuandaa wataalamu mahiri wenye uelewa mpana wa masuala ya kimataifa, amani, usalama na maendeleo endelevu.

Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim (CFR) kimejijengea sifa ya kuwa chuo cha kipekee kinachotoa mafunzo ya vitendo na kitaaluma katika nyanja za diplomasia, siasa za kimataifa na uongozi, huku kikihudumia wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali.

Mahafali hayo yanatarajiwa kuwa kilele cha mafanikio kwa wahitimu pamoja na uthibitisho wa mchango wa kituo hicho katika kuimarisha nafasi ya Tanzania katika masuala ya diplomasia na uhusiano wa kimataifa.

Post a Comment

0 Comments