TIA YASIMAMA IMARA KUTOKOMEZA CHEATING, YALINDA UBORA WA ELIMU








Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Chuo cha Usimamizi wa Biashara Tanzania (TIA) kinaendelea kudhihirisha dhamira yake ya dhati ya kulinda ubora wa elimu, uadilifu wa mitihani na thamani ya vyeti vinavyotolewa chuoni hapo kupitia utekelezaji wa ANTI-CHEATING CAMPAIGN 2025, kampeni inayolenga kumjenga mwanafunzi mwenye maarifa, nidhamu na ushindani katika soko la ajira.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika leo Januari 2, 2025, Examination Officer wa TIA Dar es Salaam alisema chuo kimeweka mifumo madhubuti ya kudhibiti vitendo vya udanganyifu katika mitihani, hatua inayolenga kulinda hadhi ya chuo na kuhakikisha haki na usawa kwa wanafunzi wote.

Alieleza kuwa katika Semester One, wanafunzi 108 walibainika kufanya cheating, idadi iliyopungua hadi 98 wakati wa mitihani ya Special na Supplementary, huku wanafunzi 101 wakikamatwa kwa kosa hilo katika Semester ya Pili. Aidha, alisema kuwa zaidi ya wanafunzi 374 waliondolewa chuoni mwaka jana kutokana na vitendo vya udanganyifu, jambo linalothibitisha msimamo thabiti wa TIA katika kusimamia maadili ya kitaaluma.

Examination Officer huyo aliongeza kuwa mitihani ya TIA husahihishwa na wasahihishaji watano tofauti, hatua inayoongeza uwazi, haki na uaminifu katika utoaji wa matokeo, huku taratibu za mitihani zikiendelea kuboreshwa ili kuziba mianya yote ya cheating.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Wanafunzi TIA, Bi. Lucina Comino, alisema kampeni hiyo inalenga kuwasaidia wanafunzi kujitambua mapema kuhusu malengo yao ya kielimu na wajibu wao kama wanafunzi wa elimu ya juu.

“Hakuna anayekuja hapa kuchukua degree tu. Unakuja kusoma programme ya miaka mitatu, siyo kuigeuza miaka sita kwa uzembe au cheating,” alisema Bi. Lucina Comino.

Aliwataka wanafunzi kujipanga, kuwa na nidhamu na kutumia vyema fursa ya elimu wanayoipata, akisisitiza kuwa idadi ya zaidi ya wanafunzi 300 kufeli au kuondolewa kila mwaka si jambo la kawaida wala la kufumbiwa macho.

“Kampeni hii itaendelea kuwabaini na kuwasaidia wale wote ambao hawajajitambua. Wazazi wanalia, wanalipa ada, lakini watoto wanafeli na hawarudi nyumbani,” alisema.

Bi. Lucina Comino alifafanua kuwa lengo la TIA si kuwaadhibu wanafunzi bali kuwawezesha kufikia malengo yao ya kitaaluma, huku akisisitiza kuwa hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa mujibu wa taratibu dhidi ya watakaobainika kufanya cheating.

“Tuko tayari kuweka wazi matukio ya cheating ili iwe funzo kwa wengine. Tunataka kuona ufaulu wa A na B+, kataa C. Huu ndiyo mpango wetu wa kuwasaidia wanafunzi wafikie ndoto zao,” alisisitiza.

Alihitimisha kwa kuwahimiza wanafunzi kuzingatia nidhamu ya mitihani na maandalizi ya mapema, akisema, “Usiende kwenye chumba cha mtihani ukiwa umechelewa. Wahi, jiandae na heshimu taratibu za mitihani.”

Kupitia ANTI-CHEATING CAMPAIGN 2025, TIA inaendelea kujijengea sifa kama chuo kinachothamini uadilifu, ubora wa elimu na mustakabali wa wanafunzi wake, kwa lengo la kuzalisha wahitimu wenye uwezo, maadili na mchango chanya kwa maendeleo ya taifa.

Post a Comment

0 Comments