Mkoani Manyara – Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, ameanza rasmi ziara ya kutembelea kaya kwa kaya katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo, anza kuhamasisha wananchi kujiunga na mpango mpya wa bima ya afya kwa wote.

Akizungumza na wananchi, Bi. Sendiga amesema mpango huu ni utekelezaji wa dira ya Serikali ya Awamu ya Sita, unaolenga kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wananchi wote bila ubaguzi.

“Kila kaya italipia shilingi 150,000 kwa mwaka, na bima hii itahudumia watu sita wa familia moja kwa kipindi cha mwaka mzima,” amesema Bi. Sendiga, akisisitiza faida za mpango huo kwa familia nyingi.

Mpango wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote (Universal Health Insurance Act, 2023) umeanza rasmi, baada ya Wakuu wa Mikoa kote nchini kuanza kusimamia usajili wa kaya maskini. Kwa awamu ya kwanza, kaya 276,000 zimechaguliwa kujaribu mfumo huu, kabla ya makundi mengine kuanza kujiunga.

Ziara ya Bi. Sendiga inalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa bima ya afya na kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa kila Mtanzania kwa gharama nafuu, huku ikichangia kuhakikisha hakuna mtu anayebaki nje ya huduma za afya.