Umoja wa wafanyabiashara wa Tanzania wanaofanya biashara Dubai ujulikanao kama TANFORD, umefanya mkutano na waandishi wa habari leo tarehe 28 Januari, 2026, jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kutangaza Kongamano la Kimataifa la Wafanyabiashara litakalofanyika Dubai tarehe 13 na 14 Februari, 2026.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa TANFORD, Hussein Jamal, amesema lengo kuu la umoja huo ni kuunganisha nguvu ya wafanyabiashara binafsi, kutetea maslahi yao, pamoja na kuleta manufaa kwa taifa na sekta binafsi kwa ujumla.
Ameeleza kuwa TANFORD inalenga kuunganisha wafanyabiashara wanaotumia kampuni zilizopo chini ya umoja huo na kuhakikisha wanapata ulinzi wa kibiashara pamoja na utetezi wa maslahi yao katika masoko ya kimataifa.
Hussein Jamal amesema kongamano hilo maalumu la kimataifa litawakutanisha wafanyabiashara, wawekezaji na wadau wa sekta binafsi kutoka mataifa mbalimbali, likiwa na lengo la kuimarisha biashara za kimataifa na mifumo ya usafirishaji na upokeaji wa mizigo kupitia Tanzania.
Amebainisha kuwa Watanzania wana nafasi kubwa ya kupeleka bidhaa zao katika masoko ya UAE, hususan Dubai, akisisitiza kuwa kongamano hilo litatoa jukwaa muhimu la kupanga na kuendesha biashara za kimataifa kwa ufanisi zaidi.
Kwa upande wake, Mgeni Rasmi katika mkutano huo amesema kuwa dunia ya sasa inahitaji ufahamu wa soko (market intelligence), akisisitiza kuwa wafanyabiashara wanapaswa kwenda moja kwa moja sokoni (field) badala ya kutegemea taarifa zisizothibitishwa.
Ameeleza kuwa sekta ya logistics na usafirishaji ni sekta kubwa na muhimu kwa Tanzania, hasa ikizingatiwa kuwa Dubai ni mji mkuu wa biashara wa Falme za Kiarabu, unaohudumia zaidi ya watu milioni nne na kuwa soko lenye mvuto mkubwa kwa wafanyabiashara na wafanyakazi.
Amesema soko la Dubai lina mchango mkubwa katika kuongeza uaminifu (credibility) wa biashara, huku sekta ya logistics ikitajwa kuwa daraja muhimu kati ya wafanyabiashara na masoko ya kimataifa.
Aidha, amewapongeza wadau mbalimbali wakiwemo ATCL, TPSF, na Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA) kwa kushiriki na kuunga mkono jitihada hizo.
Akizungumza kwa niaba ya TAFFA, Bw. Urio, amesema kuwa kwa kushirikiana na TANFORD, wameona umuhimu wa kufungua fursa kwa Watanzania ili waweze kukutana moja kwa moja na wazalishaji pamoja na wawekezaji wa kimataifa.
Ameeleza kuwa sekta ya logistics na transport imekuwa ikiongoza katika ukusanyaji wa fedha za kigeni na ina mchango mkubwa katika uchumi wa taifa, huku ikibadilika kwa kasi kubwa siku hadi siku.
Bw. Urio ametoa mfano kuwa mwezi Desemba, kampuni ya DP World ilishusha shehena zaidi ya TEUs 36,000, jambo linaloonesha ongezeko la fursa za kibiashara na ukuaji wa shughuli za bandari.
Amesisitiza kuwa fursa hizo zinaongezeka kijiografia na kuwataka wanachama zaidi ya 1,400 wa TAFFA kuzitumia kujitangaza na kukuza biashara zao, huku akiwashukuru TANTRADE na wadau wengine kwa ushirikiano wao.

0 Comments