![]() |
Na: OWM - TAMISEMI
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Dkt. Jafar Seif, ametoa wito kwa watendaji walio chini ya Ofisi hiyo kutokuwa sehemu ya migogoro katika jamii wanayoihudumia ili waweze kutenda haki wanapotoa maamuzi ya utatuzi wa migogoro.
Naibu Waziri Dkt. Seif ametoa rai hiyo leo Machi 7, 2026, alipokuwa akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Nalasi, Wilaya ya Tunduru, mkoani Ruvuma, katika mkutano wa hadhara uliolenga kujadili changamoto za mgogoro wa ardhi kati ya wakulima na wafugaji katika tarafa hiyo.
Katika maelekezo yake kwa watendaji, amesisitiza kuwa wataalam waliopo katika ngazi za chini lazima wawe mstari wa mbele katika kutatua kero za wananchi katika maeneo yao akiwataka kutokuwa sehemu ya upande wowote katika migogoro hiyo ili waweze kutoa maamuzi yasiyo na upendeleo, yasiyo na uonevu na yasiyotiliwa shaka na yeyote.
Katika mkutano huo, baadhi ya wananchi waliopata nafasi ya kueleza dukuduku zao akiwemo mwenyekiti wa Halmashauri ya Tunduru Seif Dauda wameiomba Serikali kuharakisha mchakato wa kuigawa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ili kupatikane halmashauri mbili, wakidai wilaya hiyo kongwe iliyoanzishwa mwaka 1905 ina eneo kubwa la kijiografia lenye ukubwa wa takribani kilometa za mraba 18,700, ambazo zinadaiwa kutatiza uwezo wa viongozi kutatua kero zao kwa wakati.
Akijibu hoja hiyo, Dkt. Seif amesema tayari serikali imeendelea kujenga miundombinu wezeshi katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Tunduru ili kuwahudumia wananchi wa Nalasi na maeneo mengine na kusisitiza kuwa suala hilo tayari limejadiliwa katika vikao vya ushauri vya mkoa (RCC)na taratibu za kiserikali zinaendelea, na pindi zitakapokamilika wananchi watapewa taarifa kuhusu uwezekano wa kugawanywa kwa halmashauri hiyo au hatua nyingine zinazohittajika kuchukuliwa zaidi ili kukamilisha mchakato huo.
Katika ziara hiyo Naibu Waziri Dkt. Seif ameambatana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, ambapo ziara hiyo ni utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba aliyewataka viongozi wa wizara za kisekta kufika katika Kijiji hicho cha Nalasi ili kuzungumza na wenyeji na kuwape elimu juu ya matumizi bora ya ardhi





0 Comments