Addis Ababa, Ethiopia – UONGOZI Institute kwa kushirikiana na United Nations Economic Commission for Africa (UNECA) wanatarajia kuandaa kongamano la kikanda litakalojadili usimamizi wa madini mkakati kwa ajili ya kuimarisha viwanda vya kijani na maendeleo endelevu barani Afrika.
Kongamano hilo litafanyika Aprili 27, 2026 katika makao makuu ya UNECA jijini Addis Ababa, likiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea Mkutano wa 12 wa Kikanda wa Maendeleo Endelevu.
Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Hailemariam Dessalegn, huku wasilisho kuu likitolewa na Paul Jourdan. Kongamano hilo litawakutanisha wadau mbalimbali kutoka sekta za umma, binafsi, elimu ya juu na asasi za kiraia kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
Katika kongamano hilo, washiriki watajadili masuala ya sera, fursa na uwezo wa Afrika katika usimamizi wa madini mkakati, pamoja na njia za kuongeza thamani ya rasilimali hizo ili kuchochea ukuaji wa viwanda vya kijani na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, mjadala utaangazia umuhimu wa kuimarisha mnyororo wa thamani wa madini, kulinda mazingira, pamoja na kuhakikisha haki na maslahi ya jamii zinazozunguka maeneo ya uchimbaji zinazingatiwa.
Kwa mujibu wa waandaaji, kongamano hilo pia litatoa jukwaa la kusikiliza sauti za vijana, wanawake na jamii kwa ujumla, ili kuhakikisha ushirikishwaji mpana katika maamuzi ya maendeleo.
Lengo kuu la kongamano hilo ni kutoa mapendekezo ya kisera yatakayosaidia kuimarisha usimamizi wa madini mkakati barani Afrika na kuchochea maendeleo jumuishi na endelevu.
UONGOZI Institute ni taasisi ya kikanda iliyo chini ya Ofisi ya Rais wa Tanzania, iliyoanzishwa mwaka 2010 kwa lengo la kukuza uongozi kupitia mafunzo, tafiti, mijadala ya kisera na ushauri wa kitaalamu.

0 Comments