SERIKALI YAAHIDI KUSHIRIKIANA NA MTAWADA

 



Na Nancy Mawole 


SERIKALI imeahidi kushirikiana na Taasisi inayojihusisha na utunzaji wa mazingira, Mtandao wa Waokota Taka Rejeshi Mkoa wa Dar es Salaam (MTAWADA), kwa kuwaunganisha na wanunuzi wa taka rejeshi ili pande zote mbili ziweze kunufaika.


Lengo kuu ni kupanua wigo wa ajira kupitia chama hicho na kuepukana na ukandamizaji unaohusisha wanunuzi wa taka rejeshi.


Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, leo jijini Dar es Salaam wakati wa Mkutano Mkuu wa MTAWADA 2025.


Aidha, Prof. Mkumbo amesema ataiunganisha Taasisi hiyo na wadau wengine ili waweze kupata vifaa vya kujikinga (kama vile barakoa na glovu) ili kuepuka magonjwa mbalimbali.


"Ninyi wote mnafanya kazi kwa kuunga mkono Serikali katika utunzaji wa mazingira, hivyo basi nitahakikisha wanunuzi wa taka rejeshi hao hawatakandamiza kiuchumi," alisema Prof. Mkumbo.


Amewahakikishia wanachama wote ulinzi wa kutosha ili waweze kufanya kazi zao kwa uhuru.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Martha Mollel, amesema kuwa wataendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu ajira zinazohusiana na utunzaji wa mazingira kupitia taka rejeshi.


Makamu Mwenyekiti wa MTAWADA, Said Said, amesema kuwa Taasisi hiyo imepata mafanikio makubwa, ikiwa ni pamoja na kupata wanachama 1,000 na kufungua matawi 26 katika kila mtaa wa Dar es Salaam.

Post a Comment

0 Comments