Dar es Salaam | Desemba 12, 2025
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile, ameitaka Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kuendelea kuimarisha ubunifu, tafiti za kisayansi na matumizi ya teknolojia ya kisasa ili kukabiliana na changamoto zinazolikabili sekta ya bahari na kuongeza mchango wake katika kukuza Uchumi wa Buluu nchini.
Akizungumza wakati wa Mahafali ya 21 ya DMI yaliyofanyika Desemba 12, 2025, katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, Mhe. Kihenzile amesema Tanzania ina fursa kubwa ya kunufaika na rasilimali za bahari endapo kutakuwepo na uwekezaji makini katika elimu, utafiti na ubunifu unaoendana na mahitaji ya soko la ajira la sasa na la baadaye.
Ameeleza kuwa sekta ya bahari ni miongoni mwa sekta zenye uwezo mkubwa wa kuchangia pato la taifa kupitia usafirishaji wa majini, uvuvi wa kisasa, utalii wa bahari, ujenzi wa meli na huduma mbalimbali zinazohusiana na bandari, hivyo ni muhimu kuandaa wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu.
Naibu Waziri huyo amesisitiza kuwa DMI inapaswa kuendelea kuboresha mitaala yake ili iendane na maendeleo ya sayansi na teknolojia duniani, pamoja na kuongeza tafiti zitakazosaidia kutatua changamoto halisi za sekta ya bahari nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Aidha, ametoa wito kwa uongozi wa chuo kuhakikisha miradi ya upanuzi na uboreshaji wa miundombinu inakamilika kwa wakati, akibainisha kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutaongeza uwezo wa chuo kudahili wanafunzi wengi zaidi na kutoa mafunzo yenye viwango vya kimataifa.
Katika hatua nyingine, Mhe. Kihenzile ameelekeza Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) pamoja na Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO) kushirikiana kwa karibu na taasisi za elimu ya bahari, hususan DMI, ili kutoa kipaumbele cha ajira na mafunzo kwa vitendo kwa Watanzania wenye sifa stahiki, hatua itakayoongeza ushiriki wa wazawa katika shughuli za uchumi wa bahari.
Akiwahutubia wahitimu, Naibu Waziri huyo amewataka kutumia maarifa waliyoyapata kwa ubunifu, nidhamu, uzalendo na bidii, akisisitiza kuwa vijana ni nguzo muhimu ya utekelezaji wa ajenda ya Uchumi wa Buluu na maendeleo endelevu ya taifa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam, Prof. Tumaini Gurumo, amesema chuo hicho kinakabiliwa na changamoto ya upungufu wa meli ya kisasa ya mafunzo, akieleza kuwa upatikanaji wa meli yenye uwezo wa kubeba angalau wanafunzi 200 kwa mwaka utaimarisha mafunzo ya vitendo na kuongeza ushindani wa wahitimu wa DMI katika soko la ajira.
Prof. Gurumo ameongeza kuwa DMI itaendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wa sekta ya bahari ili kuhakikisha chuo kinachangia kikamilifu katika utekelezaji wa sera na mikakati ya maendeleo ya Uchumi wa Buluu nchini.
Katika mahafali hayo, jumla ya wahitimu 2,076 wametunukiwa vyeti vya ngazi mbalimbali, wakiwemo wahitimu 78 wa Shahada ya Uzamili, 592 wa Shahada, 374 wa Stashahada, 446 wa Astashahada, 538 wa Astashahada ya Awali pamoja na wahitimu 48 wa Vyeti vya Umahiri (CoC).
Kati ya wahitimu hao, 512 ni wanawake, sawa na asilimia 20, hali inayotajwa kuwa ishara chanya ya kuongezeka kwa ushiriki wa wanawake katika elimu na shughuli za sekta ya bahari, jambo linaloendana na juhudi za Serikali katika kuhakikisha usawa wa kijinsia kwenye fursa za elimu na ajira



0 Comments