PROF. TUMAINI GURUMO: DMI YAJIPANGA KUONGOZA MAPINDUZI YA ELIMU YA BAHARI NCHINI













Dar es Salaam | Desemba 12, 2025


Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), Prof. Tumaini Gurumo, amesema chuo hicho kimejipanga kikamilifu kuongoza mapinduzi ya elimu ya bahari nchini kupitia matumizi ya teknolojia ya kisasa, tafiti bunifu na mafunzo ya vitendo, hatua inayolenga kuzalisha wataalamu mahiri watakaokuwa nguzo ya kukuza Uchumi wa Buluu na maendeleo endelevu ya taifa.


Akizungumza wakati wa Mahafali ya 21 ya DMI yaliyofanyika Desemba 12, 2025 katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, Prof. Gurumo amesema DMI ina nafasi ya kipekee katika kuandaa rasilimali watu itakayoiwezesha Tanzania kunufaika kikamilifu na rasilimali zake za bahari, zikiwemo sekta za usafirishaji wa majini, uvuvi wa kisasa, bandari, ujenzi na ukarabati wa meli pamoja na huduma nyingine muhimu katika uchumi wa bahari.


Prof. Gurumo ameeleza kuwa chuo hicho kimeendelea kuboresha mitaala yake ili iendane na mabadiliko ya sayansi na teknolojia duniani, huku kikiweka mkazo mkubwa katika mafunzo ya vitendo, ubunifu na utafiti unaolenga kutoa suluhu za changamoto halisi zinazojitokeza katika sekta ya bahari nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki.


Ameongeza kuwa licha ya mafanikio yaliyofikiwa katika miaka ya hivi karibuni, bado kuna changamoto za miundombinu ya mafunzo ya vitendo, hususan hitaji la meli ya kisasa ya mafunzo. Prof. Gurumo amesema upatikanaji wa meli hiyo utaimarisha sana ubora wa mafunzo, kuwajengea wanafunzi ujuzi wa vitendo na kuongeza ushindani wao katika soko la ajira la ndani na kimataifa.


Aidha, amesema DMI itaendelea kushirikiana na Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo ili kuimarisha miundombinu ya kufundishia, vifaa vya kisasa vya mafunzo na tafiti, pamoja na kuongeza uwezo wa wakufunzi, kwa lengo la kulifanya chuo hicho kuwa kituo cha ubora wa elimu ya bahari katika ukanda wa Afrika.


Akizungumza kuhusu dhamira ya chuo katika kukuza maadili na uzalendo, Prof. Gurumo amewataka wanafunzi na wahitimu kutumia elimu yao kwa nidhamu, ubunifu na uwajibikaji, akisisitiza kuwa maendeleo ya sekta ya bahari yanapaswa kwenda sambamba na ulinzi wa mazingira na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari.


Amesema DMI itaendelea kuwa mshirika muhimu wa taifa katika utekelezaji wa mikakati ya kitaifa ya kukuza Uchumi wa Buluu, kwa kuhakikisha elimu inayotolewa inalenga kutatua changamoto za sasa na za baadaye za sekta ya bahari, huku ikizingatia viwango vya kimataifa na mahitaji ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Tanzania.



Post a Comment

0 Comments