PROF. TUMAINI GURUMO ATAJA UHITAJI WA KUIMARISHA TEKNOLOJIA NA UBUNIFU KATIKA ELIMU YA BAHARI

 










Dar es Salaam | Desemba 12, 2025


Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), Prof. Tumaini Gurumo, amesema chuo hicho kinaendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia ya kisasa, tafiti bunifu na mafunzo ya vitendo ili kuzalisha wataalamu wenye uwezo wa kushindana katika sekta ya bahari ndani na nje ya nchi, sambamba na mahitaji ya kukuza Uchumi wa Buluu nchini.


Akizungumza wakati wa Mahafali ya 21 ya DMI yaliyofanyika Desemba 12, 2025, katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, Prof. Gurumo amesema DMI ina jukumu kubwa la kuandaa rasilimali watu itakayochangia kikamilifu katika maendeleo ya sekta ya bahari, ikiwemo usafirishaji wa majini, uvuvi wa kisasa, bandari, ujenzi wa meli na huduma zinazohusiana na uchumi wa bahari.


Prof. Gurumo amesema licha ya mafanikio yaliyofikiwa, chuo hicho kinakabiliwa na changamoto ya upungufu wa meli ya kisasa ya mafunzo, akisisitiza kuwa upatikanaji wa meli yenye uwezo wa kubeba angalau wanafunzi 200 kwa mwaka utaongeza ubora wa mafunzo ya vitendo na kupanua fursa za ajira kwa vijana.


Ameongeza kuwa DMI itaendelea kuboresha mitaala yake ili iendane na mabadiliko ya sayansi na teknolojia duniani, pamoja na kuongeza tafiti zitakazosaidia kutatua changamoto halisi zinazojitokeza katika sekta ya bahari nchini.


Akihitimisha hotuba yake, Prof. Gurumo ametoa wito kwa Serikali na wadau wa sekta ya bahari kuendelea kuiunga mkono DMI katika juhudi za kuboresha miundombinu, vifaa vya kisasa na rasilimali watu, ili chuo kiweze kutekeleza kikamilifu majukumu yake ya kitaifa na kikanda.


Katika mahafali hayo, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile, amesema Serikali inaendelea kuweka mkazo katika kukuza Uchumi wa Buluu kupitia uwekezaji katika elimu, tafiti na matumizi ya teknolojia ya kisasa.


Mhe. Kihenzile ameitaka DMI kuendelea kuimarisha ubunifu na mafunzo yenye ubora, akisisitiza kuwa maendeleo endelevu ya sekta ya bahari yanategemea uwepo wa wataalamu wenye ujuzi wa kisasa na maadili ya kazi.


Post a Comment

0 Comments