Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, leo Desemba 10 amezungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, akiweka bayana hatua kubwa zilizofikiwa katika utekelezaji wa mageuzi ya sekta ya elimu chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Prof. Mkenda, ambaye ni waziri wa pili kuzungumza na wanahabari kufuatia Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo, amesema msingi wa maendeleo ya taifa unategemea “watu, siasa safi na uongozi bora,” akibainisha kuwa Rais Samia ameongeza kwa kiwango kikubwa uwekezaji kwenye sekta ya elimu ili kuandaa rasilimali watu wenye ujuzi na maarifa ya kisasa.
Akizungumzia mikopo ya elimu ya juu, Waziri Mkenda amesema kuwa wakati Rais Samia anaingia madarakani kiwango cha mikopo kilikuwa shilingi bilioni 464, lakini kwa sasa kimeongezeka hadi takribani bilioni 900. “Huu ni uthibitisho wa dhamira ya serikali kuhakikisha vijana wanapata nafasi ya kusoma na kufikia malengo yao,” alisema.
Aidha, amesema serikali imejenga VETA za mikoa mpya katika Songwe na Simiyu, huku ujenzi wa VETA 64 ukiendelea nchini kote ili kuhakikisha kila wilaya inakuwa na kituo cha mafunzo ya ufundi. Kwa upande wa ada, ameeleza kuwa mwanafunzi anayesoma akiwa anaenda kutoka nyumbani atalipa shilingi 60,000 huku wanaokaa hosteli wakilipa shilingi 120,000.
Waziri Mkenda ameeleza pia kuwa ujenzi wa kampasi za vyuo mbalimbali unaendelea nchini kote, ambapo maeneo mengi yako hatua za mwisho kukamilika, sambamba na kuongezeka kwa bajeti ya sekta ya elimu kwa asilimia 40.
Mageuzi Makubwa ya Mfumo wa Elimu
Akieleza kuhusu mabadiliko ya mitalaa na mfumo wa elimu, Waziri Mkenda amesema mfumo wa sasa wa 7+4+2+3, uliotumika tangu miaka ya 1960, unabadilishwa rasmi chini ya uongozi wa Rais Samia. Kupitia mfumo mpya, elimu ya msingi itakuwa ya miaka 6, ambapo kila mwanafunzi atatakiwa kuendelea na elimu ya sekondari bila kukoma, hivyo kuanzisha elimu ya lazima ya miaka 10.
Kila shule ya msingi sasa itakuwa na madarasa mawili ya mwisho kwa pamoja (Darasa la 6 na 7), na kutakuwa na mahafali kwa madarasa yote hayo. Pia, umri wa kuanza darasa la kwanza utabaki kuwa miaka 6.
Waziri huyo amesisitiza kuwa mabadiliko mapya yanazingatia mahitaji ya dunia ya sasa, ikiwemo utandawazi na maendeleo ya teknolojia. Katika mtaala mpya, kila mwanafunzi wa kidato cha kwanza atalazimika kusoma somo la biashara ili kuwajengea uwezo wa kujua masuala kama TIN number na BRELA, huku somo la Kiingereza likianza kufundishwa rasmi kuanzia darasa la kwanza.
Mikondo Miwili ya Sekondari: Elimu ya Jumla na Elimu ya Amali
Kwa upande wa sekondari, serikali imeanzisha mikondo miwili—Elimu ya Jumla na Elimu ya Amali (au Ufundi). Wanaosoma Elimu ya Amali watakapomaliza Kidato cha Nne watapata cheti kinachowaruhusu kuajiriwa moja kwa moja. Serikali inaendelea kujenga shule 103 mpya za ufundi pamoja na kuweka mkakati wa kuanzisha “Politechnic Schools” mikoa ya Mwanza na Kagera.
Aidha, vyuo vya mifugo vitakuwa vikitoa Diploma pamoja na Cheti cha Form Six.
Samia Scholarship Yazidi Kufungua Milango ya Fursa
Prof. Mkenda amesema Rais Samia ameagiza kila mkoa kuwa na shule maalum za wasichana za sayansi, sambamba na kuanzisha ufadhili unaojulikana kama “Samia Scholarship” kwa vijana wenye uwezo mkubwa wa masomo. Kundi la kwanza la wanufaika 50 litaondoka mwishoni mwa Januari kuelekea Chuo Kikuu cha Johannesburg kusomea masomo ya Artificial Intelligence na Data Science, huku kundi lingine likiondoka mwezi Septemba.
Kupitia COSTECH na CRDB, serikali imetenga shilingi bilioni 2.3 kwa ajili ya kuwasaidia vijana wabunifu wanaotaka kusomea nje na kurejea kuchangia maendeleo ya taifa.
Pia, Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu itaendelea kutolewa kila Aprili 13 ikiwa ni sehemu ya kukuza ubunifu nchini.


0 Comments