Mwenyekiti wa Mradi wa Tanzania Creators Awards, Zakayo Shushu, ametangaza kuanzishwa kwa tuzo hizo maalum zitakazolenga kuwatambua, kuwathamini na kuwapa motisha watengeneza maudhui (content creators) wanaotoa mchango chanya katika jamii ya Watanzania.
Akizungumza kuhusu mradi huo, Zakayo Shushu amesema Tanzania ipo kwenye kipindi ambacho watengeneza maudhui wamekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii kwa kuhabarisha, kuburudisha, kuelimisha na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia majukwaa ya kidijitali.
Ameeleza kuwa kupitia content creators, ajira nyingi zimeweza kuundwa na biashara mbalimbali kufanyiwa matangazo, hali inayothibitisha kuwa utengenezaji wa maudhui kwa sasa ni ajira kamili inayotegemewa na vijana wengi.
“Tukasema ni muhimu kuwapa moyo content creators wanaohabarisha, wanaoburudisha na kuelimisha jamii. Ndiyo maana tumekuja na mradi wa Tanzania Creators Awards ili kupima na kuthamini thamani yao,” amesema Zakayo.
Kwa mujibu wake, tuzo hizo hazitaangalia tu umaarufu wa mtengeneza maudhui, bali zitazingatia kwa kina thamani (value) na athari (impact) ya kazi zao kwa jamii.
“Nyenzo yetu kuu siyo content yenyewe, bali kile kilichomo ndani ya content hiyo na athari ambayo mtu ameiacha kwenye jamii yake,” ameongeza.
Zakayo Shushu amesema lengo la mradi huo ni kuunda jukwaa la kitaifa litakalotambua content creators wanaotumia mchango wao kwa njia chanya, wakiwemo wanaoburudisha, wanaotoa taarifa sahihi na wanaoelimisha jamii.


0 Comments