CHATANDA AWAHIMIZA WANAWAKE KUCHANGAMKIA FURSA ZA KIUCHUMI

 




Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania Taifa, Mary Pius Chatanda, amewahimiza wanawake nchini kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi zinazotolewa na Serikali ili kujikomboa kiuchumi na kuchangia maendeleo ya taifa.

Akizungumza leo Machi 6, 2026 katika kongamano la wanawake lililoandaliwa na Umoja wa Wanawake Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam, Chatanda alisema siku ya wanawake duniani ni muhimu kwa kutambua mchango wa wanawake katika maendeleo ya jamii.

Alisema dunia ilitambua kuwa usawa wa kijinsia si anasa bali ni msingi muhimu wa maendeleo ya jamii. Alikumbusha kuwa katika historia ya kimataifa, mkutano wa wanawake uliofanyika Beijing mwaka 1995 uliweka msingi wa wanawake kudai haki zao katika vyombo vya maamuzi.

Chatanda alieleza kuwa hatua kubwa imepatikana nchini Tanzania baada ya nchi kuwa na Rais mwanamke, Samia Suluhu Hassan, aliyeshinda uchaguzi kwa asilimia 97.6 ya kura.

Alisema takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 34 ya nafasi za uteuzi serikalini zimechukuliwa na wanawake, hali ambayo ni ishara ya mageuzi makubwa katika jamii.

Akitoa mfano wa kauli ya Nelson Mandela, Chatanda alisema kumpa mwanamke nafasi ni kuwekeza katika mustakabali wa taifa.

Aidha, alisema Rais Samia aliahidi kutenga zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kuwawezesha wanawake kiuchumi, huku pia katika sekta ya manunuzi kupitia Public Procurement Regulatory Authority vikundi vya wanawake vikitengewa asilimia 30 ya fursa za zabuni.

Aliongeza kuwa Serikali imefungua mifuko mbalimbali ya kiuchumi kwa ajili ya wanawake ili kuwawezesha kujitegemea. Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 65 ya wanawake nchini wanajihusisha na shughuli za kilimo.

Katika sekta ya afya, alisema zahanati nyingi zimejengwa na kusababisha kupungua kwa vifo vya wajawazito kutoka 400 hadi 250 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Vilevile alisema mimba za utotoni zimepungua huku serikali ikiendelea kujenga shule nyingi za sayansi kwa watoto wa kike katika mikoa mbalimbali nchini.

Chatanda alisisitiza kuwa wanawake wako mstari wa mbele katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, usindikaji na teknolojia, na kuwataka wanawake kufanya kazi kwa bidii ili kuendelea kuleta maendeleo.

“Wanawake ni nguzo ya taifa. Tukiwainua wanawake, tutakuwa tumeinua taifa letu,” alisema.

Pia aliwataka wanawake kuendelea kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan ili aendelee kuiongoza nchi kwa mafanikio makubwa zaidi.

Kongamano hilo la “Wanawake Nguvu ya Jamii” limefanyika katika Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam na kuwahusisha wanawake kutoka serikalini, sekta binafsi, wajasiriamali pamoja na wanafunzi wa vyuo vikuu.

Post a Comment

0 Comments